Jumanne, 5 Aprili 2016

Maumivu ya Tumbo Wakati wa Hedhi & Vyakula vinavyopunguza mauvimu wakati wa hedhi

Maumivu ya Tumbo Wakati wa Hedhi &

Vyakula vinavyopunguza mauvimu wakati wa hedhi

Maumivu ya tumbo chini ya kitovu husumbua wasichana na wanawake wengi wakati wa hedhi zao. Maumivu haya yanaweza kuwa kidogo au wakati mwingine kuwa makali sana kiasi cha kumfanya ashindwe kufanya shughuli nyingine.
Maumivu ya Tumbo Yanavyotokea
Maumivu haya hutoka kwenye tumbo la uzazi. Wakati wa hedhi ukuta wa mji wa mimba huanza kubomoka na kisha kusababisha damu kutoka. Wakati ukibomoka misuli ya tumbo la uzazi hukaza na kusinyaa, kukaza huku ndiko kunakosababisha maumivu wakati wa hedhi.
Licha ya maumivu haya kusababishwa  na kukaza kwa tumbo la uzazi, kuna magonjwa mengine yanaweza kuchangia kuleta hali hii. Mara nyingi maumivu ya namna hii huwa makali zaidi kiasi cha kumfanya mtu ashindwe kuendelea na shughuli zake. Hali kama;
Endometriosis (uwepo wa tishu za ukuta wa mji wa mimba sehemu nyingine kama kwenye ovari au misuli ya mji wa mimba)
PID (Maambukizi kwenye via vya ndani vya uzazi)
huweza kuchangia kuleta hali hii.
Matibabu
Matibabu ya hali hii inategemea na kiasi cha maumivu. Kama maumivu ni kidogo, yanaweza kuvumiliwa na baada ya hedhi kuisha. Njia nyingine za kupunguza maumivu wakati wa hedhi;
  • Kukanda tumbo kwa maji ya moto
  • Kunywa kinywaji chenye moto
  • Usinywe vinywaji vyenye caffeine kwa wingi kama kahawa
  • Tumia dawa za kuzuia maumivu kama Paracetamol au Buscopan.

Unapoona unapata maumivu makali sana ni vizuri uonane na mtaalamu wa afya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.


Vyakula vinavyopunguza mauvimu wakati wa hedhi


Kuna baadhi ya wanawake ambao hupata maumivu tofauti wakati wa siku za hedhi kila mwezi. Maumivu  haya makali na mateso tosha kabisa kuvuruga ratiba zao za kazi, kulea familia na hata kuacha kufanya shughuli za kujiingizia kipato. Wengi hutumia dawa na kupata nafuu, wengine hawapendi dawa maana huleta madhara yasiyotegemewa mwilini na kulazimika kuvumilia mateso hadi yanapoisha.
Leo katika Makala yetu tunaangalia jinsi ya kupunguza maumivu ya hedhi kwa kuangalia vyakula mbadala vinavyoweza kutumika kama dawa. Vyakula ni njia mbadala sababu hutumika kupunguza kiwango cha homoni au kemikali zinazopekelea kuleta mauvimu mwilini.
Ili kuwa na uelewa mzuri, tuangalie kiini cha tatizo hadi kupelekea maumivu Makati wakati wa hedhi, halafu tuangalie vyakula vinavyoweza kutatua tatizo.

1. Chanzo cha maumivu

Utafiti unaonyesha kuwa kemikali aina ya prostaglandins ndio chanzo cha maumivu wakati wa hedhi kwa wanawake. Kemikali hii hutengenezwa na chembechembe za mafuta yapatikanayo kwenye seli. Kazi ya kemikali hii ni kusababisha uvimbe, kusinyaa kwa misuli, kusinyaa kwa mishipa ya damu, kuganda kwa damu, na maumivu.
Muda mfupi kabla ya kuanza hedhi, ukuta wa seli zinazotengeneza prostaglandins hujijenga kwenye mji wa mimba. Wakati wa hedhi, seli hizi hubomoka na kusababisha prostaglandins kutoka kwa wingi. Hii husababisha mishipa ya damu kusinyaa, misuli kubana na kupelekea maumivu makali. Kemikali za prostaglandins huingia pia kwenye mfumo wa damu na kusababisha maumivu ya kichwa, kizunguzungu, kichefuchefu, kutapika na kuharisha.
Kiwango cha prostaglandins ni kikubwa sana kwa wanawake wanaopata maumivu wakati wa hedhi kuliko wale wasiopata maumivu. Dawa zinazoshauriwa wakati wa hedhi, mfano: Ibuprofen (Motrin), au naproxen (Aleve), hufanya kazi ya kupunguza kiwango cha prostaglandins mwilini.
Wanawake wengi wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango hupunguza pia maumivu ya hedhi sababu vidonge huzuia ukuaji wa seli zinazozalisha prostaglandins. Lakini inawezekana pia kufikia malengo kwa kuangalia aina za vyakula.

2. Vyakula vinavyopunguza maumivu

Vyakula vinaweza kufanya kazi ya kupunguza mauvimu ya hedhi kwa kurekebisha kiwango cha homoni ya oestrogen mwilini. Oestrogen ni homoni ya kike inayotolewa mwilini kwa shughuli za kuzalisha seli. Oestrogen hutolewa kwa viwango tofauti kutegemeana na muda wa mzunguko wa mwanamke - huzalishwa kwa wingi sana baada ya hedhi na muda mfupi kabla ya hedhi kuanza.
Ili kuweza kupunguza maumivu, ni vizuri kuzingatia:
  • Punguza vyakula vyenye mafuta. Vyakula vya mafuta husababisha oestrogen izalishwe kwa wingi, hivyo kuzalisha seli nyizi zaidi kwenye mji wa mimba.
  • Kula vyakula vyenye nyuzinyuzi (fiber). Nyuzi nyuzi husaidia kusafisha mwili kwa kuondoa oestrogen kirahisi toka mwilini, hivyo kupunguza kiwango chake kwenye damu na kuzuia kukua kwa seli kwenye mji wa uzazi.
  • Acha kula vyakuja jamii ya nyama. Vyakula jamii ya nyama havina nyuzi nyuzi (fiber) hivyo oestrogen hubaki kwa kiasi kikubwa mwilini. Pia vyakula hivi vina viwango vikubwa vya mafuta ambayo ndio chazo kikubwa cha kuzalisha kemikali za prostaglandins.
  • Kula nafaka, mboga za majani na matunda kwa wingi. Jamii hii ya vyakula ina nyuzi nyuzi (fiber) inayotumika katika kupunguza kiwango cha oestrogen mwilini.
  • Acha kula vyakula vya kusindika, visivyo asili maana huwa na mafuta mengi yanayoweza kukusababisha matatizo zaidi.
Kubadilisha vyakula inasaidia sana. Wanawake wengi hufurahia matokeo na hata kuwaza kwanini wasingefanya hili zoezi mapema. Cha muhimu kuzingatia ni kula chakula bora na kupunguza uzito wa mwili ili uwe na afya bora. Ni muhimu kuacha kabisa kula vyakula vyenye mafuta na nyama, kiwango kidogo sana cha hivi vyakula huweza kupelekea madhara makubwa wakati wa hedhi.
Ni muhimu kuzingatia kula:
  • Vyakula vya jamii ya nafaka
  • Mboga za majani
  • Matunda
Acha kabisa kula:
  • Nyama na vyote vinatokana na wanyama: maziwa, mayai, nyama, na samaki
  • Vyakula vya mafuta na aina zote za mafuta: chips, peanut butter etc
Je wewe unapata maumivu wakati wa hedhi au unafahamu jinsi ya kuondoa maumivu?

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni